Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio Manchester lalaaniwa vikali na Guterres

Shambulio Manchester lalaaniwa vikali na Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali shambulio huko Manchester, Uingereza lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 20 na wengine wengi wamejeruhiwa. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Shambulio hilo la kusikitisha lilitokea Jumatatu mwishoni mwa tamasha la muziki la mwanamuziki Ariana Grande kwenye uwanja wa Manchester ambapo mlio mzito uliripotiwa na baadaye ikaelezwa kuwa watu 22 wameuawa na wengine 59 wamejeruhiwa.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa miongoni mwao ni mtoto mwenye umri wa miaka minane ambapo kufuatia ripoti hizo Katibu Mkuu kupitia msemaji wake pamoja na kulaani vikali ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali ya Uingereza huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Ameelezea mshikamano wake na serikali akisema ni matumaini yake kuwa wahusika watafikishwa haraka mbele ya sheria.

Wakati huo huo, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kabla ya kuanza kikao chao hii leo, walitumia dakika moja kusimama kimya ili kukumbuka wahanga wa shambulio hilo nchini Uingereza.

image
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waliposimama kwa dakika moja ili kukumbuka wahanga wa shambulio la Manchester nchini Uingereza. (Picha:UN/Eskinder Debebe)