Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yahitaji fedha zaidi kusaidia wakimbizi wa Burundi

UNHCR yahitaji fedha zaidi kusaidia wakimbizi wa Burundi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limerejelea wito wake kwa wahisani kusaidia nchi zinaohifadhi wakimbizi wa Burundi kutokana na kuzidi kudorora kwa hali ya usalama na hivyo raia kuzidi kukimbia nchi yao.

Mwaka huu pekee raia 70,000 wamekimbilia nchi jirani ambako mazingira katika kambi za wakimbizi mathalani nchini Tanzania, yanazidi kuwa magumu, watoto wakishindwa kupata elimu, huku wakimbizi wanaowasili wakisema ukatili wa kingono ni moja ya sababu za kukimbia nchi yao.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, Babar Baloch amesema wamelazimika kuongeza kiwango cha fedha wanachojitaji kutoka dola milioni 214 hadi milioni 250 kutokana na ongezeko la wakimbizi..

(Sauti ya Babar)

“Fedha zinahitajika sana ili kuweza kuwapatia mahitaji ya dharura wakimbizi wapya wanaowasili na pia kusaidia wenyeji. Hadi sasa UNHCR imepokea asilimia mbili tu ya fedha zinazohitajika.”

Bwana Baloch amesema hali ya kisiasa nchini Burundi ikiendelea, idadi ya wakimbizi kutoka nchi hiyo inatarajiwa kufikia nusu milioni ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, na hivyo kufanya kuwa janga la tatu la ukimbizi kwa ukubwa barani Afrika.