Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wabahái’ wasinyanyaswe Yemen-UM

Wabahái’ wasinyanyaswe Yemen-UM

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa dini au imani Ahmed Shaheed, ameonya leo kuwa mateso dhidi ya jamii ya wabahái’ mjini Sana’a nchini Yemen yakomeshwe ikiwa ni wiki chache baada ya waamini 30 wa dini hiyo kuitwa mahakamani na wengine wakitakiwa kubadili misimamo ya imani zao.

Kwa mujibu wa taarifa ya mtaalamu huyo, mnamo Aprili 17 mwaka huu, mwendesha mashtaka wa umma alitwaita waumini hao kwa njia ya simu kufika mahakamani ilihali serikali ilitoa hati ya kukamatwa wengine 25 ambao inasemekana wameshinikizwa kubadili imani.

Bwana Ahmed  amesema unyanyasaji dhidi ya imani dini ya Bahá’í unaendelea kama sio kuwa mbaya zaidi na kuongeza kuwa haikubaliki ikiwamo vitendo vya kulengwa kwa wenye dini za makundi madogo.

Amesema familia nyingi za kundi hilo mjini Sana’a wameondoka majumbani kwao na wanaishi kwa hofu kubwa.