Serikali zipiganie haki za binadamu katika afya kwa wote

22 Mei 2017

Ripoti ya kundi la ngazi ya juu la utetezi wa afya limesema utu kwa kila mwanadamu utawezekana tu endapo serikali zitaahidi kuwekeza kwenye sekta zenye uhusiano muhimu kati ya haki za binadamu na afya hususan kwa wanawake, watoto na vijana barubaru.

Kundi hilo ambalo linajumuisha wanasiasa na wataalamu wa afya na haki za binadamu limesema ahadi nyingi zimetolewa lakini bado mamilioni ya wanawake, watoto na vijana barubaru wananyimwa haki zao za kimsingi za kibinadamu, na hivyo kusababisha vifo vinavyoweza kuzuilika, kuumia, maradhi ya mwili na akili na madhara mengine.

Vile vile wameonya kuongezeka kwa upinzani dhidi ya haki za bindamu ulimwenguni kote, hususan ubaguzi dhidi ya wahamiaji, wakimbizi, watu wa asili na masikini ambao unadhoofisha zaidi maendeleo katika kuboresha afya na ustawi kwa wote, na kusema ikiwa hatua hazitachukuliwa katika kuifanya haki za binadamu kiini kwa- na kupitia- afya, basi ajenda ya maendeleo endelevu itasalia ndoto ifikapo mwaka 2030.

Hivyo wametoa wito kwa serikali kuwekeza asilimia tano ya kipato cha taifa katika afya kwa wote.

Kundi hilo liliteuliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la afya duniani, WHO na ofisi ya haki za binadamu mwezi Mei mwaka 2016 na mmoja wa wenyeviti wenza ni Tarja Halonen, Rais wa zmani wa Finland.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud