Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za raia Yei, Sudan Kusini:UM

Kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za raia Yei, Sudan Kusini:UM

Ripoti ya Umoja wa mataifa iliyochapishwa Ijumaa inaelezea matokeo ya uchunguzi wa kina kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili mwingine uliotekelezwa kwenye mji wa Yei jimbo la Equatoria ya Kati nchini Sudan Kusini kati ya Julai 2016 na Januari 2017.

Ripoti hiyo iliyotolewa na kitengo cha haki za binadamu cha mpango wa Umoja wa mataifa Sudan Kusini (UNMISS) na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, inaorodhesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia na ukatili mwingine uliofanywa na pande zote katika mzozo wa Sudan kusini kwa misingi ya kikabila au upande wanaounga mkono katika mzozo..

Hii inajumuisha mauaji ya watu 114 yaliyotekelezwa na majeshi yanaounga mkono serikali. Kiwango cha ukatili uliofanywa na upinzani hakiko bayana kutokana na kutokuwa na fursa ya kufika katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi hayo imesema.

(SAUTI EUGENE)

"Tuliweza kubaini ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliotekelezwa na pande zote katika mzozo unaojumuisha mauaji ya raia, kukamatwa kinyume cha sheria, tumeona idadi ya visa vya ukatili na unyanyasaji wa kingono, pia uporaji na uchomaji tumeona nyumba nyingi zimechomwa moto."

Pia ripoti hiyo imebaini kwamba ukiukwaji huo na ukatili unaweza kuwa uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu na imeahidi uchunguzi zaidi.

Mambo mengine yaliyotajwa katika ripoti hiyo ni pamoja na ushahidi wa mashambulizi ya kulenga raia, mauaji, uporaji, ubakaji, na uchomaji wa nyumba na majengo ya bisha, hali iliyowafanywa maelfu ya watu kufungasha virago.