Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa watoto uwe nguzo ya mikakati ya utalii katika Jamhuri ya Dominica – mtaalam wa UM

Ulinzi wa watoto uwe nguzo ya mikakati ya utalii katika Jamhuri ya Dominica – mtaalam wa UM

Watalii wanaokwenda Jamhuri ya Dominica na kuwanyanyasa watoto kingono watawajibishwa kisheria kwa uhalifu wao, ameonya mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uuzaji na unyanyasaji wa watoto, Maud de Boer-Buquicchio, akihitimisha ziara yake ya kwanza nchini humo.

Mtaalam huyo amesema ulinzi wa watoto ni sharti uwe nguzo ya mkakati wa serikali kuhusu utalii, na kutoa wito kwa serikali ya Jamhuri ya Dominica itoe ishara dhabiti kuwa lengo la kufikisha watalii milioni 10 ifikapo mwaka 2022 halitotimizwa kwa kuwaweka watoto katika hatari zaidi ya kunyanyaswa kingono.

Ametoa wito kwa Wizara ya Utalii ijumuishe uzuiaji wa baa la unyanyasaji wa watoto kingono katika mipango yake, na kuongoza juhudi zinazoendeshwa tayari na sekta binafsi ya usafiri na utalii, na jamii zilizoathiriwa, katika kutekeleza kanuni zilizowekwa za kuwalinda watoto kutokana na unyanyasaji wa kingono katika utalii.

Amesema aghalabu lawama huziendea familia za watoto walionyanyaswa pamoja na watoto wenyewe, huku wahalifu ambao mara kwa mara huwa wanaume kutoka nchi za kigeni wakisaidiwa kukwepa sheria na kuendelea kuishi kwa uhuru.