Nishati mbadala yatamalaki kambi ya kwanza ya wakimbizi Jordan:UNHCR

17 Mei 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, leo Jumatano limewasha mtambo unaotumia nishati ya jua au sola kwenye kambi ya wakimbizi ya Azraq nchini Jordan.

Mradi huo ambao umefandhiliwa na wakfu wa IKEA wa kampeni ya kuleta mwangaza katika maisha ya wakimbizi, unaleta nishati mbadala kwa maelfu ya watu ambao wameishi kwa miaka miwili na nusu wakipata umeme kwa nadra. Pia utachangia katika mkakati wa taifa wa nishati nchini Jordan ili kufikia kuwa na nishati inayojali mazingira ifikapo mwaka 2020.

Mtambo huo utaifanya UNHCR kuweza kutoa nishati ya umeme wa jua kwa wakimbizi wa Syria 20,000 wanaoishi katika makazi takribani 5000 katika kambi ya Azraq, na kukidhi mahitaji ya nishati ya vijiji viwili vilivyounganishwa na mtambo wa taifa.

Kila familia kambini hapo sasa itaweza kuwasha televisheni, friji, kipunga upepo, kuwasha taa na kuchaji simu zao za rununu ambazo ni muhimu sana kwa maisha ya wakimbizi kuweza kuwasiliana na jamii na ndugu zao.

Mradi huo umegharimu Euro milioni 8.75 na zote zimetolewa na wakfu wa IKEA.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter