Uchumi duniani waimarika ilivyotabiriwa, lakini sivyo katika maeneo maskini zaidi – ripoti ya UM

16 Mei 2017

Ukuaji katika uchumi wa kimataifa uliongezeka katika miezi sita iliyopita kama ilivyotabiriwa, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya uchumi ulimwenguni na matarajio ya mwaka 2017, ambayo imezinduliwa leo kwenye makao yake makuu jijini New York.

Aliyewasilisha ripoti hiyo kwa waandishi habari ni Diana Alarcón, Mkuu wa kitengo cha ufuatiliaji wa katika idara ya masuala ya kiuchumi na kijamii (DESA).

“Uzalishaji wa viwanda umeimarika, biashara ya kimataifa inaibuka tena, na kwa ujumla, hisia kuhusu uchumi ni nzuri zaidi. Mazao ya jumla duniani yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 2.7 mwaka 2017, na asilimia 2.9 mwaka 2018, ikionyesha kutobadilika kwa utabiri uliotolewa mnamo mwezi Januari mwaka huu.”

Mnamo mwaka 2016, mazao hayo yaliongezeka kwa asilimia 2.3 tu.

Licha ya ukuaji huo, ukuaji katika maeneo mengi bado upo chini ya viwango vinavyohitajika katika kupiga hatua za haraka kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, kwa mujibu wa Bi. Alarcón.

“Kwa mfano, wastani wa viwango vya riziki katika maeneo kadhaa ya Afrika na Amerika Kusini vilipungua mwaka jana, na vinatarajiwa kuongezeka kidogo tum waka 2017 na 2018”

Aidha, mabadiliko ya sera za kimataifa yameongeza sintofahamu kuhusu matarajio ya biashara duniani, misaada ya maendeleo, pamoja na malengo kuhusu tabianchi, imesema ripoti kwa muhtasari.

Bwana Lenni Montiel, Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu maendeleo ya kiuchumi katika DESA, amesema kuna haja ya kuimarisha azma ya kimataifa ili kutimiza ukuaji wa kimataifa wenye usawa na endelevu, ili kuhakikisha kuwa hakuna ukanda unaoachwa nyuma.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter