Skip to main content

WFP yakaribisha mchango wa China kwa wakimbizi walioko Kenya

WFP yakaribisha mchango wa China kwa wakimbizi walioko Kenya

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP leo limekaribisha msaada wa kiasi cha dola milioni tano zilizotolewa na serikali ya China kwa ajili ya usaidizi kwa wakimbizi waishio katika kambi za wakimbizi nchini Kenya.

Taarifa ya WFP kuhusu msaada huo imesema baada ya mwaka mmoja wa punguzo la mgao wa chakula kutokana na ukosefu wa fedha, mchango huo wa China na nchi nyingine umeruhusu WFP kurejesha mgao kamili kuanzia mwezi April hadi mwezi Julai.

Kwa mujibu wa sheria za Kenya, wakimbizi hawaruhusiwi kufanya kazi nje ya kambi hivyo hutegemea WFP kwa ajili ya chakula.

Mkurugenzi Mkuu na mwakilishi wa WFP nchini Kenya, Annalisa Conte amenukuliwa akishukuru kwa msaada huo na kutoa wito wa usaidizi zaidi hususani wakati huu ambapo taifa hilo la Afrika Mashariki limethiriwa na ukame.