Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid alaani mashambulizi dhidi ya MINUSCA; ataka wahalifu wawajibishwe

Zeid alaani mashambulizi dhidi ya MINUSCA; ataka wahalifu wawajibishwe

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, ameeleza kusikitishwa na kuendelea kwa machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, pamoja na mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, ambayo yamelaaniwa pia na Baraza la Usalama.

Akihutubia waandishi wa habari mjini Geneva, msemaji wa ofisi ya Kamishna Mkuu Ravina Shamdasani amesema Zeid amesikitishwa hasa na mauaji yanayowalenga raia tangu mapigano baina ya vikundi vinavyokinzana yalipoanza Novemba 2016.

Bi Shamdasani amesema kuwa machafuko yanayoendelea siyo tu kwa misingi ya dini.

“Kuna sababu za kikabila pia. Wafulani wameshambuliwa kwa misingi ya kabila lao, siyo kwa misingi ya dini, kwa hiyo kuna sababu za kidini, sababu za kikabila na pia sababu za kiuchumi.”

Ripoti za ofisi ya haki za binadamu za hivi karibuni zimeonyesha kuwa wanaume waliojihami walitumia silaha nzito nzito kushambulia MINUSCA, na kwamba uchunguzi wa kitengo cha haki za binadamu katika MINUSCA umeonyesha kuwa kati ya Machi na Mei 2017, zaidi ya raia 121 waliuawa, pamoja na walinda amani sita.

Akilaani mashambulizi na mauaji hayo, Kamishna Zeid ametoa wito kwa viongozi wa vikundi vyenye silaha kushirikiana na MINUSCA na mamlaka za serikali katika kuwafikisha wapiganaji wao walioshiriki ukiukwaji wa haki za binadamu mbele ya sheria.