Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres amteua Ovais kama Naibu Katibu Mtendaji wa UNFCC

Guterres amteua Ovais kama Naibu Katibu Mtendaji wa UNFCC

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amemteua Ovais Sarmad kutoka India kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC, katika ngazi ya Katibu Mkuu Msaidizi, imesema taarifa ya msemaji wake hii leo.

Ripoti hiyo imesema bwana Sarmad ambaye hadi sasa alishika wadhfa wa Mnadhimu Mkuu kwa Mkurungenzi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, analeta uzoefu wa miaka 27 kutoka shirika hilo, ambako mchango wake katika sera na usimamizi wa maeneo kadhaa uliimarisha kazi za IOM. Imesema mchango wake mkubwa zaidi ulikuwa katika uanzishwaji wa Ofisi ya Maadili ndani ya shirika hilo na mmoja wa washawishi katika mazungumzo ya mkataba ambao ulifanikiwa kujumuisha IOM katika mfumo wa Umoja wa Mataifa mwaka jana.

Bwana Sarmad anachukua nafasi ya Richard Kinley wa Canada ambaye aliongoza kamati hiyo kwa miaka 20.

Katibu Mkuu ametoa shukurani zake za dhati kwa bwana Kinley kwa huduma yake ya kujitolea katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.