Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umaskini waathiri asilimia 25 ya watoto Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini- UNICEF

Umaskini waathiri asilimia 25 ya watoto Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini- UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema umaskini unaendelea kuathiri zaidi ya watoto milioni 29 huko Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.

Utafiti wa UNICEF uliochapishwa hii leo umesema idadi hiyo inamaanisha kwamba mtoto mmoja kati ya wanne kwenye ukanda huo anakabiliwa na umaskini.

Watafiti walitumia vigezo vya mahitaji muhimu ya msingi kama vile elimu bora, afya, lishe na maji safi na salama ili kubaini iwapo mtoto anakosa mahitaji mawili au zaidi kati ya hayo.

Walibaini kuwa nusu ya watoto walio kwenye ukanda huo wa Mashariki ya Kati na Afrika kaskazini wana malazi duni na hawana chanzo kamilifu.

Tamara Kummer, afisa wa UNICEF katika ukanda huo akizungumza kutoka Amman, Jordan amesema..

(Sauti ya Tamara)

“Nchi katika ukanda huo hazifanyi tathmini ya mara kwa mara ya umaskini miongoni mwa watoto.  Na bila tathmini hiyo inakuwa si rahisi kutunga sera thabiti zinazoweza kushughulikia ipasavyo tatizo, chanzo chake na hatimaye kupatia suluhu suala la umaskini kwa watoto.”