Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni muhimu kushirikiana malengo ya maendeleo:Guterres

Ni muhimu kushirikiana malengo ya maendeleo:Guterres

Akizungumza jumapili katika kongamano la kimataifa mjini Beijing China, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, amefananisha mradi wa China ujulikanao kama “Ukanda mmoja, Barabara Moja” na malengo ya maendeleo endelevu SDG’s akisema , vyote mzizi wake ni maono ya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya dunia.

Amesema  vyote viwili vinajitahidi kuunda fursa, huduma bora kwa umma na ushindi katika ushirikiano vikiwa na lengo la kuimarisha 'kuunganishwa' miongoni mwa nchi na kanda, katika miundombinu, biashara, fedha, sera na, pengine muhimu zaidi ya yote, ni miongoni mwa watu.

(SAUTI GUTERRES)

Kwa mukhtada huo mradi wa ukanda na barabara unafursa kubwa ukienda Asia, Afrika na Ulaya na kuenea dunia nzima, unafika mbali kwa matamanio na kijiografia. Kwa nchi zinazotaka kuunganishwa zaidi katika uchumi wa dunia unaweza kuchagiza fursa za masoko na kufungua milango mipya. Wakati mradi huo wa ukanda na barabara na ajenda ya 2030 vinatofautiana  kwa asili na ukubwa wake vyote kitovu chake ni malengo ya maendeleo endelevu.”

Guterres amesisitiza hayo katika kongamano hilo lililohudhuriwa na Rais wa Uchina Xi Jinping na viongzi wengine kutoka nchi zaidi ya 60. Mradi huo wa “Ukanda na Barabara” ulianzishwa na China mwaka 2013 ili kuchagiza biashara na ukuaji wa uchumi katika nchi za ukanda wa Hariri na zaidi.

Guterres amesema ili nchi zote shiriki ziweze kufaidika na mradi huo ni muhimu kuimarisha uwiano uliopo baina ya mradi huo na SDG’s.

Mradi huo umearifiwa kujumisha takriban dola trilioni moja za uwekezaji wa miundombinu kwa Afrika, Asia na Ulaya. Miundombinu hiyo ni pamoja na madaraja, vinu vya nyuklia na reli.

Katibu Mkuu pia amewataka wahisani kuendelea kuwekeza katika maendeleo kupitia usaidizi rasmi (ODA) na kutimiza ahadi zao chini ya mpango wa hatua wa Addis Ababa.

Tangu alipowasili China Mei 13 Guterres amekutana na maafisa wa serikali akiwemo waziri wa mambo ya nje Wang Yi na kuwa na mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki.