Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kundi lenye sialaha lashambulia raia CAR, mlinda amani auawa:UM

Kundi lenye sialaha lashambulia raia CAR, mlinda amani auawa:UM

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR kimepeleka askari kuongeza nguvu Kusini Mashariki mwa mji wa Bangassou, ambako kundi la watu wenye silaha waliwafyatulia raia risasi usiku wa kuamkia leo na kuua idadi isiyojulikana akiwemo mlinda amani mmoja wa Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA iliyotolewa Jumamosi inasema makundi yenye silaha yanaendela kushambulia makao makuu ya MINUSCA kwa makusudi yakiwa na silaha nzitonzito ili kuwabughudhi walinda amani waache kutekeleza jukumu lao la msingi ambalo ni kullinda raia na kuokoa maisha.

Mpango huo umesema wafuasi wa muungano wa makundi likiwemo anti-Balaka walishambulia raia usiku wakiwalenga hasa Waislamu katika kitongoji cha Tokoyo mjini Bangassou.

Licha ya mashambulizi makali yaliyoelekezwa kwa MINUSCA, walinda amani walijaribu kukabiliana na mashambulizi ili kuwalinda raia katika mapigano yaliyoendelea hadi asuhbuhi ya Mei 13, ambapo mlinda amani mmoja kutoka Morocco aliuawa kutokana na majeraha ya risasi

Taarifa za awali zinasema raia waliotawanywa na mashambulizi hayo awamekimbilia msikitini, katika kanisa Katoliki na hospitali.

Kwa mujibu wa MINUSCA hivi sasa ni vigumu kusema hali ya kibinadamu mjini Bangassou, hata hivyo duru zinazoaminika zimethibitisha kuwa na idadi ya raia waliouawa na kujeruhiwa.