Jitihada za kimataifa zahitajika kukabili mabadiliko ya haraka Arctic na Antarctic

15 Mei 2017

Kampeni mpya ya kimataifa inayolenga kuboresha utabiri wa hali ya hewa, hali ya tabianchi na barafu katika maeneo ya Arctic na Antarctic imezinduliwa leo na Shirika la Hali ya Hewa (WMO), ikilenga kupunguza hali zilizo hatarishi kwa mazingira.

Aidha, kampeni hiyo inalenga kutumia vyema fursa zinazotokana na mabadiliko kasi ya tabianchi katika maeneo hayo ya ncha za kaskazini na kusini mwa sayari dunia, pamoja na kuziba mianya iliyopo sasa katika uwezo wa kutabiri hali ya hewa katika maeneo hayo.

Kampeni inakuja wakati unapoanza mwaka wa utabiri kuhusu maeneo hayo ya ncha za dunia, ambao ni kuanzia katikati ya 2017 hadi katikati ya 2019, ukijumuisha WMO na taasisi ya Kijerumani ya Alfred Wegener (AWI), na wadau wengine wengi duniani.

Katika kipindi cha miaka miwili ijayo, mtando mkubwa wa wanasayansi wa kimataifa na vituo vya utabiri wa hali ya hewa, watashirikiana katika shughuli za kufuatilia na kuchapisha matukio katika maeneo ya Arctic na Antarctic. Kwa kufanya hivyo, utabiri bora wa hali ya hewa na barafu ya bahari utapunguza hali ya hatari katika siku zijazo na usimamizi wa usalama katika maeneo hayo, pamoja na kuboresha utabiri katika maeneo ya latitudi wanakoishi watu wengi.

Kampeni inakuja siku chache baada ya WMO kupatiwa hadhi ya uangalizi katika baraza la nchi zilizoko ncha ya kaskazini mwa dunia, Arctic, zikiwemo Canada, Denmark, Finland, Iceland, Norway, Urusi, Sweden na Marekani pamoja na watu wa asili kwenye maeneo hayo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter