Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Familia zaendelea kufungasha virago Mosul kukimbia mapigano

Familia zaendelea kufungasha virago Mosul kukimbia mapigano

Hali mjini Mosul ni ya kuhaha na inazidi kuwa mbaya kwa mujibu ya wanaokimbia mji huo uliozingirwa wa Iraq.

Shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limesema Ijumaa kwamba familia hizo zimeripoti kuhusu mashambulizi ya mabomu na mapigano makubwa Magharibi mwa mji ambako wapiganaji wa ISIL wanatoa upinzani mkali kwa vikosi vya serikali.

Baadhi ya raia wamefanikiwa kutoroka kwa mujibu wa msemaji wa Andrej Mahecic

(SAUTI YA MAHECIC)

“Wamesema tumeondoka wakati mapigano yakiendelea vichwani mwetu, makombora, mashambulizi ya walenga shabaha na kadhalika. Tulifanikiwa kutoroka bila kuonekana kwa kutumia mashimo kwenye kuta za mlango wa pili ambayo yametengenezwa katika mtaa mzima. Kukimbia ilikuwa vigumu, mke wangu alimbeba binti yetu wa miezi minane nami nikambeba binti yetu mwingine. Ilikuwa vigumu sana tuliona maiti nyingi njiani na wakati mmoja mke wangu alizirahi, na hata sasa watoto wangu wanapata majinamizi, wanaamka na kulia.”

UNHCR imefungua kambi ya 12 ya wakimbizi wa ndani nje ya Mosoul lakini imeonya kwamba ukata wa ufadhili unatishia uwezo wa kambi hiyo kusaidia wakimbizi. Watu 630,000 wamekimbia Mosoul tangu kuanza kwa operesheni za kijeshi kuukomboa mji huo Oktoba mwaka jana.