Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa 69 wa WMO waendelea Geneva

Mkutano wa 69 wa WMO waendelea Geneva

Mkutano wa mwaka wa baraza tendaji la shirika la hali ya hewa duniani, WMO ulioanza jana huko Geneva, Uswisi unalenga kuimarisha huduma za hali ya hewa ulimwenguni na hivyo basi kulinda maisha ya binadamu, mali na uchumi dhidi ya hali za kupitiliza za hali ya hewa zinazokabili dunia hivi sasa.

Ikiwa ni mkutano wa 69, mkutano huo utakaomalizika tarehe 17 mwezi huu pia utatoa fursa ya kusaidia kubadilisha mchango wa shirika hilo katika ajenda ya maendeleo endelevu duniani, SDGs ya kupunguza athari za majanga na kuleta maendeleo endelevu.

Mathalani wajumbe watazindua mwaka wa kutabiri hali ya hewa kwenye maeneo yenye baridi zaidi, ikiwa ni jitihada za pamoja za kimataifa za kuimarisha utabiri wa hali ya hewa na kiwango cha barafu kwenye ncha za kaskazini na kusini mwa dunia.

WMO inasema hali mbaya ya hewa na umbali wa maeneo hayo, imesababisha hali ya hewa katika maeneo hayo ya Arctic na Antarctica kuwa maeneo yasiyofuatiliwa zaidi hali zao za hewa wakati huu ambapo jamii imekuwa na hamu kubwa ya kutembelea maeneo hayo.

Kwa mantiki hiyo uzinduzi huo utatoa fursa ya kufahamu hali ya hewa na kuweka mazingira bora ya watu wanaotaka kuyatembelea.