Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yajitahidi kumaliza mvutano baina ya Bor na Murle

UNMISS yajitahidi kumaliza mvutano baina ya Bor na Murle

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umesema unasaidia juhudi za kumaliza uhasama baina ya jamii za Dinka-Bor na Murle katika jimbo la Jonglei.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Juba Alhamisi, mkuu wa UNMISS, David Shearer amesema anatambua juhudi zinazofanywa na serikali, hususani ziara ya makamu wa kwanza wa Rais kwenye njimbo hilo na kusema UNMISS inashirikiana na viongozi wa Boma na Jonglei kutatua mzozo huo uliosababishwa na utekaji wa watoto na wizi wa ng’ombe.

(SAUTI YA SHEARER )

 “Tunahofia kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama eneo la Bor- Pibor kati ya vijana wa Dinka Bor na vijana wa  Murle.  Tumekuwa tukijihusisha na jamii huko kwa wiki mbili zilizopita na wakati huu tunapozungumza tunaunga mkono juhudi za amani za serikali na makamu wa kwanza wa Rais kuzungumza na jamii zote na kuwapa msaada wa helkopta watu hao ili waweze kuzuru jamii hizo mbili na kupunguza mvutano.

 Na kuhusu Aburoc bwana Shearer amesema wahudumu wa misaada ya kibinadamu 50 wako huko  ili kutoa msaada  kwa maelfu ya raia waliotawanywa na mapigano ya karibuni kwenye ukingo wa Magharibi wa mto Nile.

Ameongeza kuwa UNMISS imepeleka walinda amani Aburoc wiki iliyopita ili kuwezesha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu ambapo hali ya wakimbizi wa ndani inatia wasiwasi

(SAUTI YA SHEARER )

  “Tunakadiria kwamba takriban watu elfu 30 hadi 35 au pengine elfu 40 wako huko wakati huu , na wiki iliyopita tulikuwa na wasiwasi kuhusu hali yao, na kwa sababu hiyo na hususani ukosefu wa maji safi tumepeleka walinda amani . Na walinda amani hao watakuwepo huko kwa muda kutoa usaidizi ili wahudumu wa misaada ya kibinadamu  waweze kufika pia.”