Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na Benki ya Dunia zaongeza juhudi za kutokomeza njaa na umaskini

FAO na Benki ya Dunia zaongeza juhudi za kutokomeza njaa na umaskini

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Benki ya Dunia, zimetia leo saini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wao katika kutokomeza njaa na umaskini katika ngazi za kimatiafa na kitaifa.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliyotiwa saini jijini Roma, Italia, mashirika hayo mawili yatashirikiana kwa karibu kuunga mkono nchi wanachama katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), kuboresha maisha vijijini, kuimarisha ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa chakula, na kuhakikisha usimamizi endelevu wa mali asili kote duniani.

Makubaliano hayo ya kimkakati yaliyotiwa saini na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO kuhusu utendaji Daniel Gustafson, na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kuhusu sera za utendaji na huduma kwenye ngazi za kitaifa, Hartwig Schafer, yanatoa nyenzo mpya za kutekeleza ushirikiano huo, ambazo zitatumiwa katika kutoa mafunzo ya kitaaluma kwa serikali katika kuendesha miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.