Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM waitaka India irejeshe intaneti na mitandao ya kijamii Jammu na Kashmir

Wataalam wa UM waitaka India irejeshe intaneti na mitandao ya kijamii Jammu na Kashmir

India ni sharti ikomeshe mara moja marufuku dhidi ya mitandao ya kijamii ya mawasiliano na huduma ya intaneti kwenye simu za rununu katika jimbo la Jammu na Kashmir, wamesema wataalam wawili wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu.

Aidha, wataalam hao David Kaye anayehusika na uhuru wa kujieleza na Michel Forst anayehusika na hali ya watetezi wa haki za binadamu, wameitaka serikali ya India kuhakikisha uhuru wa raia wake wa kujieleza unalindwa.

Mnamo Aprili 17, serikali ya India ilipiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii na intaneti kufuatia maandamano ya wanafunzi, ikiwafungia raia wake tovuti na apu 22, zikiwemo WhatsApp, Facebook na Twitter, pamoja na huduma za data za 3G na 4G zinazotumiwa na simu za rununu na ala nyinginezo za mawasiliano.

Wamesema vizuizi hivyo kwa mawasiliano vinaathiri kwa kiasi kikubwa haki za kila mtu Kashmir, na hivyo kudunisha dhamira ya serikali ya kuzuia kuenezwa kwa taarifa zinazoweza kuchangia machafuko.