Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapishi wakimbizi kuonyesha vipaji vyao Ulaya

Wapishi wakimbizi kuonyesha vipaji vyao Ulaya

Mradi uliozinduliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR na wadau wengine wa kuonyesha vipaji vya wapishi wakimbizi kwa lengo la kuwajumuisha katika jamii na kuwawezesha umezidi kushika kasi na kusambaa katika miji 13 barani Ulaya. Amina Hassan na ripoti kamili.

(Taarifa ya Amina)

Mradi ulizinduliwa mwaka jana ambapo kuanzia tarehe 15 hadi 30 mwezi Juni mwaka huu, wakimbizi wenye stadi za upishi wataonyesha stadi zao wakati wa tamasha lijulikanalo kama “Tamasha la Chakula la Wakimbizi".

Wakati wa tamasha hilo, migahawa zaidi ya 50 itafungua majiko yao kwa ajili ya wapishi wakuu wakimbizi kutoka Somalia, Syria, Ukraine, Eritrea, Afghanistan na maeneo mengine.

UNHCR imesema mafanikio makubwa ya mradi huo barani humo yametokana na wito wa ulimwengu kutaka kuiga tamasha hilo katika nchi zao.

Mradi huo umesaidia kuleta wakimbizi na wananchi karibu zaidi katika mazingira bora ya kiutamaduni, ikiwa ni maandalizi ya mlo mzuri na kufurahia chakula bora, kukuza vipaji vyao na kupata ajira, na fursa kwa wananchi kugundua mila na desturi zingine na kwa wakimbizi kugundua utamaduni mpya.

Kwa mantiki hiyo UNHCR na Shirika lisilo la Kiserikali la Food Sweet Food limeandaa vipeperushi kwa wale wanaotaka kuandaa tamasha hilo katika miji yao.