Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kura turufu isitumike kwenye masuala ya mauaji- Jopo

Kura turufu isitumike kwenye masuala ya mauaji- Jopo

Kundi huru la viongozi wastaafu wa Umoja wa Mataifa limetaka kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa na marekebisho ya muundo wa umoja huo ili kukidhi mahitaji ya sasa.

Wakizungumza kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani viongozi hao wanaopigia chepuo amani na haki za binadamu duniani wamesema changamoto za sasa ni kubwa kwa nchi moja kuweza kuhimili.

Naibu Mwenyekiti wa kundi hilo Gro Harlem Brundtland, ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu wa Norway akasema ni kwa mantiki hiyo ushirikiano wa kimataifa unahitajika huku akienda mbali zaidi kuzungumzia matumizi ya kura turufu kwa nchi zenye ujumbe wa kudumu wa Baraza la Usalamala Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Brundtland)

“Bado tunahisi kwa uthabiti kabisa kuwa kuna umuhimu wa kujizuia kutumia kura turufu kwenye suala linalohusisha mauaji ya kikatili ya watu wengi na pia dalili za kuwepo kwa mauaji ya aina hiyo.”

Mary Robinson, ambaye ni rais mstaafu wa Ireland na Kamishna mkuu mstaafu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa aliangazia suala la haki za binadamu akisema..

(Sauti ya Robinson)

“Ni jambo la kushtusha kuwa katika karne ya 21 kuna vikwazo vingi. Haki za binadamu na heshima kwa haki za wakimbizi na wahamiaji ikiwemo wale wanaongia kwenye nchi bila vibali. Bado wote wana haki na haki zao lazima ziheshimiwe.”

Kundi hilo la wazee lilipatiwa mamlaka hiyo na Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela na linaongozwa na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan likiwa na jumla ya wajumbe wengine 10.