Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yahaha kusaidia Yemen na Sudan Kusini kukabili kipindupindu

IOM yahaha kusaidia Yemen na Sudan Kusini kukabili kipindupindu

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM linaendelea kusaidia Sudan Kusini na Yemen kukabiliana na magonjwa ya kuhara na kipindupindu wakati huu ambapo kipindupindu kimebainika pia miongoni mwa wahamiaji huko Yemen.

Mathalani nchini Yemen, IOM imetoa msaada wa dawa na vifaa vya matibabu kwenye hospitali ya Al-Jumhori mjini Sana’a, kufuatia kuthibitishwa kwa visa vya kipindupindu wakati huu ambapo vita nchini humo imesambaratisha vituo 274 vya afya. Joel Millman ni msemaji wa IOM huko Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Millman)

“IOM katika miezi sita iliyopita imechunguza dalili za kipindupindu kwa wahamiaji 36,000 nchini Yemen ambapo visa Tisa vimethibitishwa kwenye kundi hilo huko Aden na Hudaida. Ingawa hali ya usalama si nzuri, wafanyakazi wetu wanaendelea kufuatilia mlipuko.. Idadi inaonekana siyo kubwa lakini inaongezeka.”

Nchini Sudan Kusini hali ya kipindupindu ni mbaya zaidi huko Jiech, kwenye kambi za wakimbizi wa ndani zinazojumuisha binadamu na wanyama ambapo IOM imeanzisha vituo vitatu vya kuwapatia wananchi maji ya kuongeza nguvu mwili sambamba na kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga.