Bensouda ataka hatua dhidi ya magendo ya wahamiaji Libya; Saif Gaddafi ahamishiwe ICC

Bensouda ataka hatua dhidi ya magendo ya wahamiaji Libya; Saif Gaddafi ahamishiwe ICC

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) Fatou Bensouda, amesema hali tete ya usalama iliyoshamiri nchini Libya imechangia utekelezaji wa uhalifu mbaya sana, akitaja ripoti za mauaji ya raia, utekaji nyara, vizuizi vya holela, utesaji na ukatili wa kingono.

Akilihutubia Baraza la Usalama leo alasiri kuhusu hali nchini Libya, Bi Bensouda amesema ofisi yake inaendelea kukusanya na kufanyia tathmini taarifa za uhalifu unaotendwa dhidi ya wahamiaji wanaojaribu kuvuka kupitia Libya.

“Ninasikitishwa sana na ripoti kuwa maelfu ya wahamiaji, wakiwemo wanawake na watoto, wanashikiliwa vizuizini nchini Libya, aghalabu katika mazingira duni. Ukiukaji, ukiwemo mauaji, ubakaji na utesaji, unadaiwa kuenea.”

Bi Bensouda amesema amepokea taarifa za kusikitisha kuwa Libya imegeuzwa soko la usafirishaji haramu wa binadamu. Kwa mantiki hiyo, ametangaza kuwa ofisi yake inatathmini uwezekano wa kufungua uchunguzi katika makosa yanayohusiana na usafirishaji haramu wa wahamiaji nchini humo, iwapo masharti ya mamlaka ya mahakama hiyo yatatimizwa.

“Baraza hili lenyewe limeeleza wasiwasi wake kuwa hali nchini Libya inazidi kuzorota kwa sababu ya magendo na usafirishaji haramu wa wahamiaji wanaoingizwa, wanaopitia au wanaotokea Libya. Vitendo hivi huenda vikaweka mazingira yanayofanya mitandao ya uhalifu wa kupangwa na ugaidi kunawiri.”

Akizungumza kuhusu haki kufuatia matukio ya wakati wa mapinduzi, Bi Bensouda amesema ofisi yake imepokea taarifa kuwa Saif Al-Islam Gaddafi, mwanae aliyekuwa rais wa Libya Muammar Gaddafi, hayupo tena chini ya ulinzi wa Bwana At-‘Ajami al-‘Atiri, kamanda wa kikundi cha wanamgambo cha Zintan, na kwamba sasa yupo chini ya ulinzi wa Baraza la Kijeshi la Zintan.

“Natoa wito kwa serikali ya makubaliano ya kitaifa ichukue hatua stahiki kumhamishia Bwana Gaddafi chini ya ulinzi wake ili Libya iweze kumhamishia kwa Mahakama ya ICC, kulingana na wajibu wake chini ya sheria ya kimataifa.”