Fursa na ufadhili vyahitajika kuinusuru Yemen-UM

8 Mei 2017

Pande kinzani katika mzozo wa Yemen zimetakiwa kuhakikisha zinatoa fursa haraka na bila masharti wala vikwazo kuweza kuwafikia maelfu ya watu wanaohitaji msaada.

Wito huo umetolewa na Jamie McGoldrick mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen akizungumzia hofu kutokana na ukosefu wa fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu kama dawa, na vifaa vya afya nchini humo.

Ameongeza kuwa kuwapa fursa bila masharti Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu kuwafikia wahitaji kutaonyesha dhamira ya pande hasimu kwa maslahi ya watu wa Yemen.

Kwa mujibu wa taarifa ya McGoldrick iliyotolewa Jumapili ucheleweshwaji katika viwanja vya ndege, vituo vya upekuzi na kuingilia usafirishaji wa misaada kumeathiri juhudi za kusafirisha kwa wakati muafaka dawa na vifaa vingine vya matibabu kwa watu wanaovihitaji.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa fursa kwa sasa ni muhimu zaidi ukizingatia kuna tishio la baa la njaa na mlipuko wa kipindupindu katika maeneo mbalimbali nchini humo. Watu milioni 17 wanakabiliwa na uhaba wa chakula na kufanya mgogoro huo ndio kuwa mkubwa kabisa wa njaa duniani.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter