Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo yasiwe chanzo cha ajali za barabarani- WHO

Maendeleo yasiwe chanzo cha ajali za barabarani- WHO

Wiki ya usalama barabarani duniani ikianza hii leo, shirika la afya duniani, WHO linasema zaidi ya watu milioni 1.2 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali za barabarani, idadi kubwa ikiwa ni barani Afrika ikifuatiwa na Amerika ya Kusini na Asia. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Ongezeko la idadi ya magari katika nchi zinazoendelea likienda sambamba na mwendokasi hata maeneo ya makazi ya watu vimetajwa kuwa sababu ya ongezeko la ajali za barabarani katika maeneo ya Afrika, Asia na Amerika Kusini.

WHO kupitia Dokta Etienne Krug ambaye ni mkurugenzi wake wa masuala ya kuzuia majeraha na magojwa yasiyo ya kuambukiza anasema miundombinu haiimarishwi kuendana na idadi ya magari na watu bila kusahau sheria za barabarani kutokusimamiwa ipasavyo hata katika maeneo ambako zimepitishwa..

(Sauti ya Etienne)

“Tunahitaji utashi wa kisiasa kwa sababu katika nchi hizi nyingi watu wanaamini kuwa hiyo ni gharama ya kulipa kwa ajili ya maendeleo. Iwapo tutaendelea, tunahitaji barabara mpya, magari mengi zaidi na hivyo kutakuwepo na vifo zaidi barabarani. Haipaswi kuwa hivyo.”

Amesema Canada na Sweden ni miongoni mwa nchi ambazo idadi ya magari imeongezeka lakini idadi ya vifo kutokana na ajali za barabarani imepungua kwa sababu wanahakikisha miundombinu ya barabarani inakidhi viwango vinavyotakiwa.

WHO imetenga wavuti maalum ambamo kwayo kuna takwimu na taarifa mbali mbali kuhusu wiki ya usalama barabarani ambayo itamalizika tarehe 14 mwezi huu.