Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yakaribisha kuachiliwa kwa watoto 82 wa Chibok

UNICEF yakaribisha kuachiliwa kwa watoto 82 wa Chibok

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, limekaribisha kuachiliwa kwa watoto 82 nchini Nigeria hapo jana Jumamosi, wahafamikao maarufu kwa jina la wasichana wa Chibok, ambao walitekwa na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Taarifa ya UNICEF imemnukuu mwakilishi wa shirika hilo nchini Nigeria Pernile Ironside, akisema kuwa wafanyakazi wa shirika hilo wameanza kutoa usaidizi wa juhudi za kuwatambua watoto walioachiliwa na kuwapa msaada wa kitabibu.

Amesema iliumiza mioyo kufahamu kuwa wasichana hao watarejea kwenye familia zao na kuongeza kuwa watoto hao watakabiliwa na mchakato mgumu na mrefu wa wa kujenga upya maisha yao, baada ya tukio la kuogofya la kutekwa nyara ambalo liliwasababishia athari za kisaokolojia.

Bi Ironside, amesema UNICEF iko tayari kusaidia mamlaka za Nigeria katika kutoa msaada yakinifu wa kisiakolojia na kuhakikisha elimu kwa watoto hao itaendelea katika mazingira salama.

UNICEF kadhalika imelitaka kudi la kigaidi la Boko Haram kukomesha machafuko dhidi ya watoto, hususani ukatili wa kingono na ndoa za mapema, na kusisitiza kuwa juhudi kuu zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha watoto hao wanakuwa salama.

Miaka miatatu iliyopita kundi la watoto 276 walitekwa na Boko Haram, na kabla  ya kuachiliwa kwa 82 Jumamosi hii, watoto 195 walikuwa wanashikiliwa.

Duru zinasema watoto walioachiwa tayari wamewasili mji mkuu wa Nigeria Abuja, na kusalimiana na Rais wa nchi hiyo Muhammadu Buhari.