Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yahimiza unawaji mikono ili kupambana na usugu wa viuavijasumu

WHO yahimiza unawaji mikono ili kupambana na usugu wa viuavijasumu

Leo Mei Tano ni siku ya usafi wa mikono, na katika kuadhimisha siku hii mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) linamulika umuhimu wa usafi wa mikono katika utoaji wa huduma za afya.

Kwa mujibu wa WHO, mmoja kati ya kila wagonjwa kumi hupata maambukizi wakati anapopata huduma ya matibabu, ambapo hadi asilimia 32 ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji hupata maambukizi ya baada ya kupasuliwa. Hadi asilimia 51 ya maambukizi hayo huwa sugu kutibiwa na viuavijasumu.

Kauli mbiu ya kampeni ya mwaka huu “Pambana na usugu wa viuavijasumu … uwezo upo mikononi mwako,” inalenga kuonyesha uhusiano muhimu kati ya kuzuia maambukizi na vitendo kama vile unawaji mikono katika kuzuia usugu wa viuavijasumu.

Kupitia kampeni ya mwaka huu, WHO inatoa wito kwa nchi na vituo vya huduma za afya viimarishe programu za kuzuia na kudhibiti maambukizi, kwa kufuata mwongozo wa WHO, ili kubadili mienendo ya watu na kupunguza kusambaa kwa maambukizi, na hivyo kuokoa uhai wa mamilioni ya watu.