Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa majaribio kuleta ahueni kwa wagonjwa wa saratani

Mradi wa majaribio kuleta ahueni kwa wagonjwa wa saratani

Shirika la afya duniani, WHO limetangaza mradi wa majaribio unaolenga kupunguza gharama za dawa zinazotumika kutibu saratani.

Mradi huo unahusisha utengenezaji wa dawa zinazofanana na zile za gharama ya juu za kutibu saratani ambapo WHO imekaribisha kampuni zinazoweza kutengeneza dawa hizo za bei nafuu kuwasilisha maombi yao.

Lengo ni kuwezesha dawa za bei ghali ambazo ni rituximab na transtuzumab zilizoko katika orodha ya dawa muhimu ya WHO, ziweze kuzalishwa kwa bei ya chini na hatimaye zitumiwe na wagonjwa katika nchi za kipato cha kati na chini.

Mkurugenzi msaidizi wa WHO Marie-Paule Kieny amesema dawa hizo ni ghali kwa kuwa hutengenezwa kwa kutumia chembechembe hai hivyo kupatikana kwa mfanano wake kutakuwa ni fursa nzuri ya kupanua wigo wa usaidizi kwa nchi ambako zinahitajika.

WHO inatarajia mradi huo kuanza kutekelezwa mwakani.