Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziarani Colombia, Baraza la Usalama lakariri uungaji wake mkono amani

Ziarani Colombia, Baraza la Usalama lakariri uungaji wake mkono amani

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wameanza leo ziara ya kihistoria nchini Colombia, ambako wamekariri kuwa uungaji wao mkono kwa dhati mchakato wa amani nchini humo, baada ya zaidi ya miaka 50 ya mgogoro.

Wajumbe hao wamepokelewa na Rais wa Colombia Juan Manuel Santos, kwenye ikulu ya nchi hiyo mjini Bogota, iitwayo jumba la Narino.. ambaye ameshukuru Umoja wa Mataifa kwa usaidizi wake katika kusimamia usitishaji mapigano.

“Usitishaji mapigano katika mzozo wowote ule ni mgumu sana kutekelezwa, lakini katika muktadha wa Colombia, umefanikiwa kweli. Tangu ulipotangazwa zaidi ya miezi minane iliyopita, hapajawa na kifo wala majeruhi kwa raia na vikosi vyetu vya jeshi kwa sababu ya kuzozana na FARC. Aidha, hapajawa na mapigano yoyote kati ya FARC na vikosi vya umma, wala utekaji nyara wowote.”

Rais huyo amewaarifu wajumbe wa Baraza la Usalama kuhusu utekelezaji wa mkataba wa amani, ambao awamu yake ya kwanza imetekelezwa kwa asilimia 75%.

Naye Rais wa Baraza la Usalama, Balozi Elbio Rosselli wa Uruguay, amesisitiza haja ya wito wa amani kwa watu wa Colombia, akisifu ujasiri wao wa kisiasa katika kuendeleza mchakato wa amani, na kwamba mchakato huo una manufaa ndani na nje ya Colombia.

“Bara la Amerika, tokea ncha ya kaskazini hadi ncha ya kusini, ndipo mahali pekee duniani ambako hakuna mgogoro unaoendelea moja kwa moja. Ndilo eneo pekee duniani.”

Akikariri uungaji mkono wa Baraza la Usalama kwa Colombia, ameongeza kuwa michakato ya amani kawaida haiendi kwenye barabara ilonyooka kwani panaweza kuwa na vikwazo, lakini kilicho muhimu zaidi ni kusalia kwenye mkondo, na kwamba Baraza hilo lina azma ya kutoa usaidizi wanaohitaji watu wa Colombia.