Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya Katibu Mkuu yaweka wazi maovu wanayotendewa watoto Nigeria

Ripoti ya Katibu Mkuu yaweka wazi maovu wanayotendewa watoto Nigeria

Ripoti mpya ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuhusu watoto na migogoro ya silaha nchini Nigeria imetaja ukiukaji mkubwa unaotekelezwa na vikundi vyenye silaha, hususan Boko Haram, na kulaani vikali vitendo hivyo. Joshua Mmali na taarifa kamili.

(Taarifa ya Joshua)

Ripoti hiyo ambayo ndiyo ya kwanza ya aina yake kuhusu hali nchini Nigeria, inajumuisha taarifa kuhusu athari za mgogoro wa silaha dhidi ya watoto kati ya Januari 2013 na Disemba 2016, ikitaja vitendo vya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya shule, utekaji nyara wa idadi kubwa ya watoto, pamoja na kutumiwa kwa wasichana katika mashambulizi ya mabomu ya kujitoa mhanga.

Ripoti inaangazia majimbo matatu kaskazini mashariki mwa Nigeria ambayo yameathirika zaidi na mgogoro wa silaha, yakiwa ni Adamawa, Borno na Yobe, ikijumuisha pia hali katika nchi jirani ambazo zimeathiriwa na mgogoro wa Boko Haram.

Pande zilizotajwa kutekeleza ukiukaji huo ni Boko Haram, vikosi vya usalama vya Nigeria na kikosi kazi cha pamoja cha raia.

Katika hitimisho la ripoti hiyo, Katibu Mkuu analaani vikali ukiukaji unaoendelea kutendwa na Boko Haram dhidi ya watoto, akisema idadi kubwa ya watoto waliouawa au kulemazwa, kutendewa ukatili wa kingono au kutumikishwa na vikundi vilivyojihami inasikitisha, na kutaka Boko Haram wakome ukiukaji huo.