Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jeshi la Côte d’Ivoire liko tayari kubeba jukumu kutoka UM

Jeshi la Côte d’Ivoire liko tayari kubeba jukumu kutoka UM

Vikosi vya usalama vya Côte d’Ivoire vimejiandaa kubeba majukumu ya ulinzi yaliyokuwa yanatekelezwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNOCI ambao unakamilisha majukumu yake tarehe 30 mwezi ujao.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Aichatou Mindaoudou, ambaye anaongoza UNOCI amesema ujumbe huo umesaidia serikali kurejesha utulivu kufuatia mzozo ulioibuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2010.

(Sauti ya Mindaoudou)

"Vikosi vya usalama vya Cote D'Ivoire viko tayari kubeba majukumu yote ya ulinzi yaliyokuwa yanatekelezwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa.”

Kuhitimishwa kwa operesheni za UNOCI ambayo imekuwemo nchini humo kwa miaka 13 unafuatia kuimarika kwa mamlaka ya serikali, taasisi za demokrasia na huduma bora za kijamii bila kusahau uchumi na marekebisho ya sekta ya  ulinzi.

image
Waliokuwa na mahitaji ya kitabibu nao pia walipata msaada kutoka kwa walinda amani wa UNOCI ambapo pichani mlinda amani kutoka Jordan akimpatia maelezo ya tiba mtoto anayeishi kwenye mazingira magumu huko Yopougon Anokoi. Matibabu kwa watoto hao yalikuwa ni ya bure. Picha: UN/Basile Zoma
Kuondoka kwa UNOCI hakufungi pazia la Umoja wa Mataifa kwa kuwa umoja huo utaendeleza ushirikiano kupitia ofisi zake za kitaifa nchini humo.

UNOCI ilianzishwa mwaka 2004 baada ya Cote D'Ivoire kugawanyika kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Uchaguzi uliokuwa  ufanyike mwaka 2005 uliahirishwa hadi mwaka 2010 ambapo rais wa wakati huo Laurent Gbagbo alikataa kukabidhi madaraka kwa mshindi wa uchaguzi Alassane Ouattara.

Takribani watu 3,000 waliuawa wakati wa vita hivyo na Ouattara kuapishwa mwezi Mei mwaka 2011.