Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yasitishwe Syria suluhu ikisakwa-de Mistura

Mapigano yasitishwe Syria suluhu ikisakwa-de Mistura

Wakati mazungumzo ya kusaka suluhu ya mgogoro wa Syria yakiendelea, Umoja wa Mataifa umeonyesha matumaini hususani katika hatua ya sitisho la mapigano, amesema mwakilishi maalum wa umoja huo kwa ajili ya Syria Staffan de Mistura.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Astana nchini Kazakhstan, kunakofanyika majadiliano hayo de Mistura amesema ana matumaini kuwa upande wa upinzani utashiriki katika mazungumzo mjini Astana na kusisitiza kuwa jambo muhimu ni kufuatilia sitisho la mapigano,akisema mara nyingi wawapo kwenye majadiliano upande mmoja hushambulia.

Katika hatua nyingine mwakilishi huyo maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, amesema umoja huo unasikititishwa kwa kile alichosema kuendelea kwa mashambulizi hususani ya anga nchini humo.

Ametaka uchunguzi wa haraka ufanyike, na hakikisho la sitisho la mapigano wakati huu ambapo majadiliano ya kukomesha kabisa machafuko nchini Syria yanaendelea.