Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu mpya wa WFP akamilisha ziara ya kwanza Syria na Lebanon

Mkuu mpya wa WFP akamilisha ziara ya kwanza Syria na Lebanon

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) David Beasley, amekamilisha ziara yake huko Syria na Lebanon, ambako amejionea moja kwa moja madhila ya watu kutokana na mgogoro wa Syria.

Katika mahojiano kufuatia ziara yake hiyo ya kwanza kabisa kama mkuu wa WFP, Bwana Beasley ameiambia Idhaa ya habari za Umoja wa Mataifa kwamba amesikitishwa kuona matatizo wanayokumbana nayo watu waliolazimika kuhama makwao Syria, na shinikizo kubwa dhidi ya jamii zinazowapa hifadhi nchini Lebanon.

Amesema mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Syria, ikiwemo WFP, yanahaha kujaribu kuweza kuwafikia watu wote wanaohitaji usaidizi nchini Syria.

“Tunawalisha takriban watu milioni nne ndani ya Syria kila mwezi, lakini bado kuna wengine milioni 4.7 walioko katika maeneo magumu kufikiwa na yaliyozingirwa na wapiganaji.”

Amesema wamefanya tathmini kuhusu takriban watu zaidi ya 640,000 wanaoishi katika maeneo 13 yaliyotenganishwa kabisa na hayafikiki.

“Tunafanya kazi na pande zote husika pamoja na viongozi katika serikali ya Syria ili kufanya tunachoweza kuwafikishia chakula watu wanaohitaji usaidizi. Hawa raia wasio na hatia wamenaswa katika mgogoro ambao hawakuanzisha wao. Huu ni mzozo ulioanzishwa na mwanadamu, na inahuzunisha sana.”

Mkuu huyo mpya wa WFP pia amehadithia madhila ya familia za Wasyria ambao amekutana nao nchini Lebanon na ndani ya Syria, akisema inavunja moyo kuona mateso wanayopitia, lakini akaongeza kuwa ameshangazwa kuona kuwa licha ya yote hayo, bado wanaonyesha uthabiti mkubwa na azma ya kuendelea kuishi.