Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyombo vya habari ni muhimu katika kuchagiza uaminifu

Vyombo vya habari ni muhimu katika kuchagiza uaminifu

Katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer leo amewatukuza waandishi wa habari wengi waliopoteza maisha yao nchini humo, mmoja wao akiwa ni John Gatluak aliyeuawa na wengine walibakwa na kunyanyaswa wakati wa mgogoro mwezi Julai mwaka jana.

Akizungumza mjini Juba nchini Sudan Kusini wakati wa maadhimisho hayo, amesema kama hiyo haitoshi, bado kuna mwaandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa ambaye yuko kizuizini na wengine wengi walifungwa na wengine bado wamefungwa, na vitendo hivyo vyote ni lazima vilaaniwe.

Halikadhalika amegusia ripoti ya kwamba serikali imefungia chombo cha habari cha Al-Jazeera-Kiingereza na kuzuia waandishi wa habari kutoka nje kuingia nchini humo...

(Sauti ya Shearer)

“Kila demokrasia ni lazima ilinde uhuru wa vyombo vya habari. Ujumbe uletwao na vyombo vya habari unaweza kuwa haushabihiani na sisi, lakini ujumbe wao ni muhimu, sawa na yote. Uwazi ndio suluhu ya kupambana na rushwa na vitendo potofu, na vyombo vya habari ni mchangiaji muhimu katika kuangaza mwanga huo juu yetu”.