Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea uchaguzi mkuu Agosti, Kenya yachukua hatua kujenga amani

Kuelekea uchaguzi mkuu Agosti, Kenya yachukua hatua kujenga amani

Serikali ya Kenya imesema imechukua hatua ili kuepusha machafuko na kauli za chuki kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Agosti mwaka huu. Amina Hassan na ripoti kamili.

(Taarifa ya Amina)

Katibu katika ofisi ya mwanasheria mkuu wa Kenya Maryann Njau-Kimani amesema hayo mbele ya wajumbe wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya kutokomeza aina zote za ubaguzi inayokutana huko Geneva, Uswisi.

Amesema suala kwamba uchaguzi mkuu unafanyika, liliibua tashwishi na hivyo serikali imechukua hatua mapema siyo tu kuepusha kauli za chuki na za kibaguzi zinazoweza kuchapishwa au kutangazwa kupitia vyombo vya habari, bali pia kushughulikia masuala yanayoleta tofauti za kijamii.

Mathalani amesema wameanzisha jukwaa la Uwiano ambalo kwamo wadau wa kitaifa na kaunti wanabadilishana taarifa kuhusu viashiria vinavyoweza kuleta uchochezi.

Hatua nyingine ni za kisheria hususan umiliki wa ardhi na kuhakikisha pia huduma za kijamii kama vile elimu zinapatikana kwa wakazi wa pembezoni, bila kusahau mfuko wa kusaidia waathirika wa visa vya kihistoria.