Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Studio maalum kuhusu SDGs yazinduliwa Geneva

Studio maalum kuhusu SDGs yazinduliwa Geneva

Huko kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi kumezinduliwa studio maalum yenye lengo la kutoa fursa kwa watu kujadiliana kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Wageni katika studio hiyo pamoja na kujadili pia wanaweza kuona kile ambacho Umoja wa Mataifa na wadau wake wamechangia kufanikisha utekelezaji wa malengo hayo 17 yaliyoridhiwa na nchi wanachama mwaka 2015.

Miongoni mwa wageni hadi sasa ni mkunga kutoka Malawi na Rais wa Chile ambapo mijadala ni pamoja na jinsi ya kutokomeza umaskini, usawa wa kijinsia na hata kulinda mazingira ya sayari dunia.

Mkuu ofisi ya Umoja wa Mataifa Geneva, Michael Møller, ambaye amebuni mradi huo amesema ni fursa kwa wataalamu kubadilishana simulizi zao na kuchochea wengine kuchukua hatua kufanikisha SDGs.

Bwana Møller alimhoji Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed kuhusu malengo ya maendeleo endelevu na mahojiano hayo na mengine yanapatikana kupitia chaneli ya Youtube www.youtube.com/SDGStudio