Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tiba kwa wahanga wa silaha za sumu hubadilika na wakati- WHO

Tiba kwa wahanga wa silaha za sumu hubadilika na wakati- WHO

Shirika la afya duniani, WHO limesema kadri milipuko ya matumizi ya kemikali za sumu inavyojitokeza, nao wanabadili mbinu za kusaidia nchi wanachama kukabiliana na madhara yatokanayo na mashambulio hayo.

Mwanasayansi wa WHO anayehusika na masuala ya usalama wa afya Dokta Maurizio Barbeschi amesema hayo leo huko Geneva, Uswisi wakati akielimisha wanahabari kuhusu jukumu la shirika hilo pindi kemikali za sumu zinapotumiwa kama silaha au kwa makusudi dhidi ya raia.

Mathalani amesema huko Iraq tangu mwezi machi mwaka huu wamebaini matumizi ya silaha za sumu zinazoharibu mishipa ya fahamu kwa hiyo usaidizi wa matibabu unakwenda na wakati kwa kuwa..

(Sauti ya Dkt. Maurizio)

“Kile kilichokuwa suluhisho bora kwa mwezi Oktoba wakati na mapigano yalikuwa Mosul kinapaswa kutathminiwa upya na msaada wetu kwa hospitali na mafunzo lazima yaende vivyo hivyo. Na katika hili tuliandaa fomu za uchunguzi na mfumo wa kiufundi kwa kiingereza na kiarabu na pia vifaa vya kujikinga.”

Amerejelea kauli ya WHO kuwa hawana wajibu wa kuchunguza nani ametumia silaha na kwa sababu zipi na badala yake shirika hilo linawabika kusaidia kwenye matibabu kwa wagonjwa na kusaidia vifaa ili kukinga wanaotoa huduma.