Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa UM kuhusu Syria kushiriki mkutano Astana

Mjumbe wa UM kuhusu Syria kushiriki mkutano Astana

Ofisi ya Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, imetangaza kuwa mjumbe huyo atashiriki mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Syria mjini Astana, kuanzia Mei tatu hadi nne.

Taaria ya ofisi hiyo imesema kuwa kufuatia haja ya dharura na umuhimu wa kuanzisha tena jitihada za kuhakikisha hali haizoroti zaidi nchini Syria na kuendeleza hatua za kujenga imani katika mchakato wa amani, Bwana de Mistura amekubali kuhudhuria mkutano huo kama mwangalizi, baada ya kualikwa na serikali ya Kazakhstan.

Akiwa Astana, mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ataunga mkono juhudi za wadhamini wa usitishaji mapigano na washiriki wengine ili kuiondoa hali tete ya kijeshi iliyopo nchini Syria.

Aidha, mjumbe huyo ambaye ataandamana na ujumbe wa wataalam wa Umoja wa Mataifa ambao wamewahi kushiriki mikutano ya awali ya Astana, ataitumia fursa hiyo kufanya mashauriano ya kisiasa na wadhamini wa usitishaji mapigano, na wengine watakaokuwepo.