Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yatoa wito wa kulinda raia Aburoc

OCHA yatoa wito wa kulinda raia Aburoc

Mratibu wa mpito kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Sudan Kusini, OCHA Serge Tissot, amezitaka pande za mzozo nchini humo zitekeleze majukumu yao ya kuwalinda maelfu ya raia wa Shilluk,  waliokimbia mapigano makali ya hivi karibuni baina ya serikali na makundi mengine magharibi mwa ukingo wa mto Nile.

Bwana Serge amesema raia hao waliosaka hifadhi katika eneo karibu na ndani ya Aburoc wanaishi kwa hofu bila kujua maslahi yao ya kesho, akitoa wito kwa serikali kuheshimu makazi hayo na kuhakikisha hawashambuliwi, na wito kwa pande kinzani kuhakiksha maeneo  yaliyojaa raia yamo na yanasalia bila ya makundi ya kijeshi.

Vile vile amewasihi wale waliopora mali za OCHA huko Aburoc kuzirejesha haraka, kwani ni vifaa vitakavyotumika kuokoa raia ambao wengi wao wametembea kwa miguu bila ya maji na chakula, wakiwasili katika eneo hilo wamechoka na wadhaifu.

Ametoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa watoa misaada, mali zao na maeneo wanakofanya kazi zinaheshimiwa na kulindwa na pia kuwaruhusu kuingia maeneo hitajika kutoa misaada bila ya vikwazo vyovyote.