Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid amulika ukiukaji wa haki za binadamu; vizuizi dhidi ya ofisi yake

Zeid amulika ukiukaji wa haki za binadamu; vizuizi dhidi ya ofisi yake

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, ameelezea masikitiko makubwa kuhusu hali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kufuatia ripoti za mauaji ya mamia ya watu na makaburi 40 ya halaiki. Taarifa kamili na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora)

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Bwana Zeid amesema wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kukusanya taarifa za ukiukaji huo wa haki kwa kuzungumza na waathiriwa, huku wakitoa shinikizo kuhakikisha wanaokiuka haki wanawajibishwa.

“Tunaomboleza vifo vya mamia ya watu ambao wameuawa miezi michache iliyopita nchini DRC, na tunatoa wito ufanywe uchunguzi huru na haki itendeke, bila kujali ni akina nani wametekeleza au kupanga mauaji hayo.”

Zeid ambaye amemulika pia hali ya haki za binadamu katika nchi zingine, zikiwemo Burundi, Sudan Kusini, na Yemen, amesema wafanyakazi wa ofisi yake wamekuwa wakikumbana na vikwazo vingi wanapotaka kufanya uchunguzi katika nchi hizo.

Amesema ukiukaji wa haki za binadamu umesababisha njaa Sudan Kusini na Yemen, huku ofisi yake ikiendelea kusotwa kidole cha lawama, kwa mfamo ikisingiziwa kuwa na njama dhidi ya serikali ya Burundi.