Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wakaribisha hatua Sahara Magharibi, mamlaka ya MINURSO yaongezwa

UM wakaribisha hatua Sahara Magharibi, mamlaka ya MINURSO yaongezwa

saharamagharibiwikendiUmoja wa Mataifa umekaribisha kujiondoa kwa wafuasi wa kundi la Frente Polisario kutoka eneo la Guerguerat kule Sahara Magharibi, kama ilivyothibitishwa na waangalizi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Sahara Magharibi (MINURSO) mnamo Aprili 27-28, 2017.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imesema kuwa hatua hiyo, ikichukuliwa pamoja na kujiondoa kwa vikundi vya Morocco kutoka eneo hilo kufuatia wito wa Katibu Mkuu, itaongeza matumaini ya kuweka mazingira yatakayowezesha utekelezaji mapema azma ya Katibu Mkuu ya kuzindua tena mchakato wa mazungumzo kwa njia mpya na moyo mpya unaozingatia mwongozo wa maazimio ya Baraza la Usalama.

Lengo hasa ni kufikia suluhu ya kisiasa inayoweza kukubaliwa na wote, na inayoweka njia ya watu wa Sahara Magharibi kujiamlia mustakhbali wao.

Aidha, taarifa hiyo imetoa wito kwa pande kinzani kutimiza wajibu wao chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano, na kuheshimu malengo yake, na kushirikiana kikamilifu na MINURSO.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu inafuatia Baraza la Usalama kupitisha azimio la kuongeza muda wa MIURSO hadi tarehe 30 Aprili 2018, na kuzitaka pande kinzani ziheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano.