Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko mapya Sudan Kusini yanaongeza mateso kwa raia – UM

Machafuko mapya Sudan Kusini yanaongeza mateso kwa raia – UM

Umoja wa Mataifa umeeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa machafuko na mateso kwa raia wa Sudan Kusini, kufuatia operesheni ya hivi karibuni ya jeshi serikali ya nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu imetoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini na pande zingine kinzani kusitisha uhasama na kutimiza wajibu wao wa kulinda raia.

Aidha, Umoja wa Mataifa umezitaka pande kinzani kushirikiana nao na wahudumu wengine wa kibinadamu ili kuhakikisha kuwa raia walioko hatarini magharibi mwa ukingo wa Mto Nile wanafikiwa salama.

Umoja wa Mataifa umesema kuongezeka upya kwa mapigano unaonyesha kupuuza kwa ahadi zilizowekwa wakati wa mkutano wa IGAD wa Machi 25 2017, za kutekeleza makubaliano ya usitishaji mapigano na kuwezesha ufikishaji misaada, na kukariri kuwa hapawezi kuwepo suluhu la kijeshi kwa mzozo wa Sudan Kusini.