Mjadala kuhusu wajibu wa kulinda kabla ya ripoti ya Katibu Mkuu

28 Aprili 2017

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kuzuia mauaji ya kimbari na wajibu wa kulinda, imekuwa na mjadala leo na nchi wanachama kuhusu suala hilo, kama sehemu ya maandalizi ya ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu wajibu wa kulinda.

Akizungumza katika mjadala huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Peter Thomson, amesema licha ya kuungwa mkono kwa ngazi za juu zaidi katika serikali, kanuni ya wajibu wa kulinda imefeli kuendelezwa vyema.

“Tumeona katika maeneo mengi duniani, kumeongezeka viashiria na hali hatarishi zinazoweza kuchangia utendaji wa uhalifu wa kikatili, mathalani migogoro, ukiukwaji wa haki za binadamu, mifumo hafifu ya serikali, ukwepaji sheria kwa wanaotenda uhalifu, mienendo ya kibaguzi, matamshi na mashambulizi yanayoyalenga makundi fulani, pamoja na sababu za kisiasa na kiuchumi zinazochochea hali hizi hatarishi kunawiri.”

Amesema dhima ya mwaka huu kuhusu uwajibikaji kwa ajili ya kuzuia ukatili ni muhimu hata zaidi, akiongeza kuwa wajibu wa kulinda ni wito kwa nchi zote kuchukua hatua zifaazo na zinazohitajika katika kuzuia uhalifu wa kikatili.

Naye Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari na wajibu wa kulinda, Adama Dieng amesema

“Tunashuhudia hali iliyoenea ambapo watu wamo hatarini kuathiriwa na uhalifu wa kikatili, ukiwemo mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu, au ambapo uhalifu huu tayari unatendeka.”

Bwana Dieng amesema hali hii inaibuka wakati ushirikiano wa kimataifa ukizidi kufifia, kudorora heshima kwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu, na migawanyiko ya kisiasa katika viungo vya uamuzi muhimu kama vile Baraza la Usalama. Ametoa wito kwa nchi za Magharibi na Ulaya zisifikirie tu kuwa wajibu wa kulinda ni suala la kigeni.

“Siku zote tunasisitiza kuwa hakuna nchi au eneo linaloweza kujiona kuwa na kinga tosha dhidi ya hatari ya uhalifu wa kikatili, na kwamba utekelezaji wa wajibu wa kulinda unapaswa kuanza kwa kila nchi kujifanyia tathmini kuhusu udhaifu wake na hali zinazoweza kufanya ukiukwaji wa haki za binadamu au sheria ya kimataifa ukageuka kuwa uhalifu wa kikatili.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter