Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya El Niño huenda ikajitokeza nusu ya pili ya 2017-WMO

Hali ya El Niño huenda ikajitokeza nusu ya pili ya 2017-WMO

Licha ya kutokuwepo na hali ya hewa ya El Niño hadi sasa mwaka huu , kuna uwezekano mkubwa wa zaidi ya asilimia 50 hali hiyo itajitokeza katika nusu ya pili ya mwaka huu wa 2017.

Onyo hilo limetolewa na shirika la kimataifa la utabiri wa hali ya hewa (WMO) siku ya Ijumaa. Hali ya hewa ya El Niño husababisha kubadilika kwa joto la bahari na kuleta mtafaruku katika maeneo mengi duniani ikiwemo joto kali ambalo husababisha mvua kubwa.

Huathiri zaidi nchi zinazoendelea na na WMO inatabiri kwamba kuanzia Juni hali ya El Niño inauwezekano mkubwa wa kutokea. Mkurugenzi wa idara ya utabiri ya WMO, Maxx Dilley, amesema kumbukumbu ingali mbichi ya matukio ya 2015-2016 yaliyohusiana na ukame, mafuriko na kuathitri miamba ya matumbawe sehemu mbalimbali duniani.

Amesema ukichanganya na mabadiliko ya tabia nchi hali hiyo imesababisha ongezeko la joto na kufanya kuwa na miaka miwili mfululizo iliyokuwa na historia ya joto kali.

Amesisitiza kuwa utabiri sahihi wa matukio utaokoa maisha na ni muhimu kusaidia kilimo, uhakika wa chakula, udhibiti wa maji, na juhudi za upunguzaji majanga.