Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu ya milioni moja walazimika kuhama makwao DRC

Zaidi ya watu ya milioni moja walazimika kuhama makwao DRC

Zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuhama makwao kufuatia miezi minane ya machafuko yanayozidi kusambaa katika majimbo ya Kasai, Lomami na Sankuru, kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, OCHA imesema Umoja wa Mataifa na wadau wake wamezindua ombi la dola milioni 64.5 ili kushughulikia mahitaji ya dharura ya kibinadamu ya watu 731,000 walioathiriwa na mzozo huo kwa kipindi cha miezi sita ijayo.

OCHA imesema idadi ya watu waliolazimika kuhama makwao ni kubwa sana katika mikoa mitano yenye idadi ya watu wapatao milioni 25. Mashirika ya kibinadamu yamo mbioni kuongeza jitihada za usaidizi katika eneo hilo ambalo awali lilikuwa tulivu katika nchi hiyo kubwa ilokumbwa na migogoro ya muda mrefu.

Jens Laerke ni msemaji wa OCHA, Geneva

“OCHA na mashirika mengine ya kimataifa yameongeza uwepo wao mashinani. Hata hivyo, tunakabuliwa na changamoto mpya inayohitaji rasilmali za ziada ili kuwasaidia watu waliofurushwa makwao na vilevile jamii zinazowapa hifadhi wanakokimbilia.”