Mafuta ya jenereta za hospitali Gaza haba; UM watoa ufadhili

27 Aprili 2017

Mratibu wa shughuli za kibinadamu na maendeleo katika Umoja wa Mataifa, Robert Piper, ameeleza kusikitishwa na hali inayoendelea kuzorota ya nishati kwenye Ukanda wa Gaza, na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa, mamlaka za Israel na Palestina zichukue hatua haraka ili kulinda utoaji huduma muhimu kwa wakazi wa Gaza milioni 1.9.

Bwana Piper ameonya kuwa huduma muhimu zipo karibu sana kukwama, kwani mafuta ya dharura karibu yanaisha, huku umeme ukiwa unakatika kwa hadi saa 20 kila siku.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, mafuta ya kuendesha jenereta za dharura katika hospitali saba kati ya 13 Gaza, yanatarajiwa kwisha katika siku tatu zijazo.

Tayari wakazi wa majengo ya ghorofa hawapokei maji, kwani hakuna nguvu za umeme za kufikisha maji ya bomba katika nyumba zilizopo juu.

Mfuko wa ufadhili kwa maeneo ya Palestina yaliyokaliwa, ukiongozwa na Bwana Piper, umeidhinisha leo dola milioni 500,000 kwa ajili ya kununulia mafuta ya dharura, ili kuendeleza huduma muhimu katika hospitali na vituo vingine vya afya.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter