Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya hati miliki: Thamani ya kulinda uvumbuzi na ujuzi yamulikwa

Siku ya hati miliki: Thamani ya kulinda uvumbuzi na ujuzi yamulikwa

Leo ni siku ya hati miliki duniani, na katika hafla ya kuadhimisha siku hii jijini Geneva, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema ujuzi unaoshikiwa bango na shirika la hati miliki duniani (WIPO) utasaidia kuamua mustakhbali wa jamii ya kimataifa.

Akihutubia wafanyakazi wa WIPO, Bwana Guterres amesema jamii ya kimataifa inakabiliana na changamoto nyingi, zikiwemo zinazohusu teknolojia mpya na masoko ya ajira yanayobadilika, ambayo yataathiri maisha ya watu. Kwa mantiki hiyo, amesema shirika la WIPO linaweza kuwa nyenzo muhimu kwa Umoja wa Mataifa unapokabiliana na changamoto hizo, kwa kutoa ujuzi kuhusu kinachoendelea, na mapendekezo ya jinsi ya kujiandaa kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo.

Mwaka huu, siku hii inaadhimishwa kwa kutizama jinsi mfumo wa hati miliki unavyosaidia uvumbuzi kwa kuvutia uwekezaji, kuwafaidi wabunifu, kuwahamasisha kuendeleza ubunifu wao, na kuhakikisha kuwa ujuzi wao utaweza kuweka msingi kwa wavumbuzi wa siku zijazo.