Tunahitaji dola milioni 64 kunusru wakazi wa Kasai-OCHA

Tunahitaji dola milioni 64 kunusru wakazi wa Kasai-OCHA

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, leo imetoa ombi la dola milioni 64.5 kwa ajili ya usadizi kwa zaidi ya watu 730,000 jimboni Kasai nchini Jmahuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC. Grace Kaneiya na taarifa kamili.

(TAARIFA YA GRACE)

Kwa mujibu wa OCHA msaada huo wa kibinadamu unahitajika kwa kipindi cha miezi sita ijayo ili kunusuru maisha ya watu hao waliotatizwa na mapigano baina ya vikosi vya serikali na wanamgambo jimboni Kasai, yaliyozuka mwezi Agosti mwaka jana.

OCHA inasema machafuko jimboni humo yamesababisha zaidi ya watu milioni moja kukosa makazi, huku pia raia kadhaa wakipoteza maisha na kuripotiwa uvunjifu wa haki za binadamu ikiwamo haki ya elimu ambapo maelfu ya watoto wamekatizwa masomo.

Ofisi hiyo ya kuratibu misaada yaa kibinadamu inasema kuwa machafuko jimboni Kasai, DRC yametatiza ustawi wa jamii kwa ujumla huku yakichochea mlipuko ya ugonjwa wa utapiamlo .

Mathalani OCHA wanasema jimboni Kasai Kati pekee, mahitaji ya sasa ya kibinadamu ni asilimia 400 zaidi ya mipango ya usaidizi kwa mwaka 2017.