Haki za maji na mazingira safi zachunguzwa Mexico

26 Aprili 2017

Mtaalamu Huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maji na Usafi wa Mazingira, Léo Hela atafanya ziara nchini Mexico Mei 2 hadi10 kuchunguza upatikanaji wa maji na mazingira safi kwa vikundi vinavyoishi katika mazingira magumu.

Amesema ziara yake katika maeneo ya Mexico City, Veracruz na Chiapas ni kutathmini upatikanaji, ufikiaji , unafuu na ubora wa maji ya kunywa na mazingira safi kwa watu wa asili, wahamiaji, watu wa mashinani, masikini na wale wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi.

Vile vile amesema atachunguza jinsi haki za binadamu za kupata maji na mazingira safi zinavyozingatiwa katika ngazi ya kitaifa na shirikisho pamoja na serikali za mitaa na kama huduma hizo zinafuata kanuni na viwango vya kimataifa.

Katika ziara hiyo atakutana na wawakilishi wa serikali, asasi za kiraia, wakaazi wa maeneo husika na mashirika mengine, na atatoa ripoti ya uchunguzi wake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu mwezi Septemba.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter